Fugwe ya Mse ni ugonjwa unaosababishwa na ukungu aina ya Sphacelotheca sorghi na hushambulia sana mtama. Mtama ulioshambuliwa na ugonjwa huu mbegu zake huwa na unga mweusi (umejaa viyoga) uliofunikwa na ngozi ngumu yenye rangi kati ya nyeupe, maziwa na kikahawia. Hii huitwa sorus/sori. Sori hutofautiana kwa ukubwa na rangi. Sori zinaweza kufikia urefu wa sentimita 1.2 na huwa na rangi kati ya nyeupe na kahawia. Viyoga (spores) hutoka nje pale ngozi inapopasuka wakati mbegu za mtama ziko katika hatua ya kukomaa mpaka kukauka. Kiasi kidogo cha suke hadi suke zima linaweza kuathiriwa. Katika mmea ulioambukizwa na ugonjwa huu, masuke yote au baadhi yake yanaweza kuwa na fugwe. Itokeapo hali hiyo, mara nyingi suke la kwanza linaweza lisishambuliwe na fugwe lakini yale yanayofuatia katika mche huo hushambuliwa. Idadi ya mimea inayoweza kuambukizwa shambani inaweza kuwa ndogo au kubwa sana kutegemea uwingi wa mbegu zilizoambukizwa na vinyoga